Saturday, November 22, 2014

Zaidi 28 wauwawa na wanamgambo Kenya

Polisi nchini Kenya wanasema kuwa wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al Shabaab wamewauwa kwa kuwapiga risasi zaidi ya watu 28 waliokuwa wakisafiri kwenye basi moja karibu na mpaka wa Somalia.
Maafisa wa ngazi ya juu wamesema kuwa basi hilo lilitekwanyara katika Jimbo la Mandera wakati likiwa njiani kuelekea katika mji mkuu Nairobi.
Watu wasiokuwa waislamu wanasemakana kutengwa na abiria wengine na kisha kupigwa risasi.
Kundi la al-Shabab nchini Somalia limetekeleza mashambulizi kadhaa nchini Kenya tangu mwaka 2011.
Huo ndio mwaka ambapo Kenya iliwatuma wanajeshi wake nchini Somalia kupigana na kundi hilo la waislamu wenye itikadi kali.
Mji wa Mandera katika eneo la Kaskazini mashariki ndio ulioathirika pakubwa. Baada ya shambulio hilo la mapema jumamosi maafisa katika eneo hilo wamenukuliwa na vyombo vya habari nchini kenya wakisema kuwa serikali ilikataa kuitikia ombi lao la kutaka usalama kudumishwa zaidi.
Afisa mmoja ameliambia gazeti la Daily Nation kwamba wavamizi hao waliwataka abiria kusoma aya katika Koran kabla ya kuwaangamiza walioshindwa kufanya hivyo.

Friday, November 21, 2014

Zambia:Kaimu rais atimuliwa chamani

Chama tawala nchini Zambia (PF) kimemtimua kaimu rais wa nchi hiyo Guys Scott kutoka chamani na kuvunja utaratibu wa katiba.
   

  Taarifa hii ni kwa mujibu wa msemaji wa chama hicho.
''Amekuwa akiwaajiri na kuwafuta watu kazi ovyo na pia bila ya kushauriana na kamati kuu ya chama,'' amesema Malozo Sichone.
Bwana Scott, ambaye licha ya hatua hiyo ataendelea kuwa mwanachama wa chama hicho, ataendelea kuhudumu kama kaimu rais hadi uchaguzi utakapofanyika tarehe 20 Januari.
Scott aliteuliwa kuwa kaimu rais kufuatia kifo cha hayati Rais Michael Sata aliyefariki mwezi jana.